Social Icons

Pages

Tuesday, February 2, 2010

FANYA HAYA BASI SIKU YA WAPENDANAO MPENDWA WANGU..


Pamoja na ukweli kwamba Valentine day ni fursa ya kuoneshana upendo na amani kwa wote bila kujali umri, jinsia na uhusiano wa kama vile kaka na dada, mama na mtoto n.k. naomba niruhusu niipe safu hii ya uwanja wa mapenzi haki yake.

Kwa wale walioshibana na kupendana kwa dhati ni nafasi yao kuweza kudhihirisha mapenzi yao kwa maneno na vitendo. Lakini kwa wale wenye mapenzi yanayolegalega, huitumia nafasi hii kufufua penzi lililopoteza matumaini ya uhai ili waweze kufurahi tena katika sayari ya mapenzi kama kawa!

Aisee, mapenzi matamu! Asikwambie mtu hasa yanapopata wenye kuyajulia hukaribia kuleta uchizi kwa kunoga kwake, lakini pia hugeuka shubiri kwa wale wanaoamua kuyakoroga kwa makusudi. Mapenzi ni sanaa, mapenzi ni utundu, ubunifu na hayataki kukurupuka.

Mpendwa wangu, usikubali siku hii ya Valentine ikupite “kavu kavu” wewe na mpenzi wako, yaani hakuna haja na hairuhusiwi kisheria kutafuta visababu vitakavyowafanya mnuniane, msemezane vibaya na kadhalika ili kupisha siku hii maalum ipite salama bila ya rabsha.

Peaneni zawadi
Zawadi, kwa lugha ya wenzetu “gift” ina maana kubwa sana katika mapenzi. Haijalishi ndogo au kubwa, pipi kijiti,maua au funguo za gari ni muhimu na ina nafasi kubwa sana katika siku kama ya leo.

Tokeni pamoja
Italeta raha wapendanao mkafanya mtoko kwa kutembelea sehemu mpya isiyozoeleka kwenu ili kuifanya siku yenu hii iwe ya kumbukumbu, kwani kubadilisha mazingira kutachochea hisia tamu za mapenzi kati yenu.

Lugha laini
Lugha laini na maneno matamu yanayotoka kwa sauti yenye mvuto wa mapenzi ni moja ya sehemu muhimu ya kuonesha hisia zako za mapenzi ya dhati kwa mwenzi wako.

Kukumbushana nyakati tamu za nyuma
Maisha ya mapenzi ni safari ndefu, kuna milima na mabonde, mafanikio na changamoto mbalimbali, matamu na machungu, lakini kwa siku maalum kama hii mnaweza kukumbushana siku ambazo mlikuwa na furaha

Tathmini ya maisha yenu
Si vibaya pia mkatumia siku hii kutathmini maendeleo yenu ya maisha ya kimapenzi na kupanga mikakati mipya itakayoimarisha penzi lenu.

Ifanyeni siku ya suluhu
Kwa wale waliokwaruzana kwenye mapenzi yao, nadhani ni siku muhimu kwao kutafuta suluhu kati yao na hatimaye kusameheana na kuanza ukurasa mpya wa mapenzi yao.

Lakini wakati huohuo, nawakumbusha wale wanaoihusisha siku hii na suala la ngono zembe bila kujali athari za janga la Ukimwi. Nawaomba waachane na ulimbukeni huo kwani mapenzi hayaishii tu kwenye ngono.

1 comment:

 1. Beres Hammond alisema "it feels GREAT to win another LOVE, but when when you lose the one closest to your heart, EVERYONE CAN HEAR YOU THINKING LOUD"
  Kwangu na mke wangu siku ya wapendano ni leo. Namaanisha KILA LEO.
  Na namshukuru Mungu kuwa naye hapendi kwa Tarehe. Nadhani siku ya Feb 14 si ya kusherehekea. Tulistahili kuwa na SIKU YA KUWAJALI WENYE UHITAJI badala ya kuibadili siku ya Feb 14 kuwa na anasa, matumizi na kuambukizana magonjwa.
  Mie SIKU YANGU NA WAKATI WA KUPENDANA NA WANGU NI SASA. Yaani sekunde hii niandikayo.
  Twapendana kwa kiduchukiduchu. Yaani penzi la kila sekunde. Si mzigo saana maana mwaka umegawiwa kwa sekunde. Sasa wale wasubiriao Feb 14 ndio watoe penzi la mwakaaaaa. Kazi kwao
  Hahahahaaaaaaaaaaaaaaaa
  Blessings Sis Kidu...
  Stay Blessed

  ReplyDelete

 

Sample text

Sample Text